Kisa cha kwanza cha Mpox katika binadamu kilitokea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mwaka wa 1970. Tangu miaka ya 1980, kumekuwa na ongezeko la polepole la idadi ya visa katika nchi fulani, hasa DRC na Nigeria. Hali hii huenda inatokana na kusitishwa kwa chanjo ya kawaida ya ndui mwaka 1980.
Mzuko wa kimataifa wa mpox (aina ndogo ya II) ulianza mwaka 2022, ambao ulienea sana kupitia ngono. Tangu 2023, kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya visa vya mpox (aina ndogo ya I) nchini DRC. Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza mzuko huo kuwa janga la kimataifa la afya ya umma tarehe 14 Agosti 2024. DRC imeathirika zaidi, lakini idadi inayoongezeka ya nchi nyingine za Afrika pia zimeathirika.
Hatari ya kuambukizwa nchini Norway ni ndogo.
Jinsi unavyoweza kuambukizwa mpox
Maambukizi kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kawaida hutokea kwa kugusana kimwili kupitia vipele na viowevu vya mwili. Kugusana kingono na mtu aliyeambukizwa huongeza hatari hii. Unaweza pia kuambukizwa kupitia matone, kama vile yale yanayosababishwa na kukohoa na kupiga chafya, lakini lazima mtu awe karibu kimwili na abakie hapo kwa muda mrefu (saa nyingi).
Uwepo wa virusi umegunduliwa katika shahawa muda mrefu baada ya mtu kupona, lakini haijulikani ikiwa hali hii inasababisha hatari ya kuambukizwa zaidi. Kwa hivyo, inashauriwa kutumia kondomu wakati wa kujamiiana kwa wiki 12 baada ya kupona.
Katika nchi za Afrika ambapo ni chanzo asili cha ugonjwa huu, virusi hivi vinaweza pia kusambazwa kutoka panya hadi kwa binadamu.
Je, unaweza kuwa umeambukizwa kwa muda gani kabla ya dalili kuonekana?
Kawaida huchukua kati ya siku 6 na 13 tangu kuambukizwa hadi kuanza kuugua (kipindi cha kuatamiza), lakini kipindi hiki hutofautiana na kinaweza kuwa kifupi au zaidi (hadi siku 21).
Unaweza tu kuwaambukiza wengine unapokuwa na dalili. Kwa maneno mengine, huwezi kuwaambukiza watu wengine wakati wa kuatamiza kabla ya ugonjwa kudhihirika.
Dalili za mpox ni gani?
Dalili za kawaida za mpox ni:
- upele na homa (zaidi ya nyuzi 38 ° C)
- kuvimba na maumivu tezi za limfu
- Maumivu ya koo
- maumivu ya kichwa
- uchovu
- maumivu ya misuli
Upele hubadilika na kuwa malengelenge, ambayo huota na kisha kukauka na kuanguka. Makovu yanaweza kutokea.
Upele kawaida huanzia kwenye sehemu ya mwili ambayo iliathiriwa na maambukizi. Kwa watu wengi walioathiriwa na mzuko huo mwaka 2022, upele ulianzia karibu na sehemu za siri na eneo la puru. Watu wengi walioambukizwa walipata malengelenge machache tu.
Upele unaweza pia kuanzia mahali pengine kwenye mwili, kama vile uso, midomo au mikono. Watu wengine pia hupata upele kwenye viganja na nyayo za miguu. Katika hali mbaya zaidi, upele unaweza pia kuenea kwenye mwili wote. Katika matukio hayo, upele unaweza kufanana na wa tetekuwanga.
Watu wengine hupata maumivu ndani na karibu na upele, ikiwa ni pamoja na katika tezi za limfu.
Watoto, wanawake wajawazito na watu walio na kingamwili dhaifu wako kwenye hatari kubwa ya kuugua sana kutokana na mpox.
Dalili kawaida huchukua wiki 2 hadi 4. Unaweza kuwaambukiza wengine kuanzia mwanzo wa dalili hadi vipele vinapoanguka na ngozi mpya kumea chini (karibu wiki 3).
Vipimo, uchunguzi na matibabu
Ikiwa umehatarishwa na maambukizi haya, unapaswa kuzingatia hasa dalili za ugonjwa uliotajwa hapa juu.
Ikiwa unashuku kuwa huenda umeambukizwa mpox, unapaswa kuepuka kugusana kimwili na watu wengine na kupata ushauri wa daktari wako. Dalili zake zinaweza kuwa sawa na magonjwa mengine mengi ya kawaida. Kwa hivyo ni muhimu upimwe na daktari, ambaye pia atashauri kama unapaswa kupimwa. Huwezi kupimwa ili kubaini kama umeambukizwa au la hadi ugonjwa udhihirike.
Watu wengi hawahitaji matibabu yoyote kando na kupunguza makali ya dalili, kama vile dawa za kupunguza homa au za kutuliza maumivu.
Visa vya ugonjwa mkali au kulazwa hospitalini ni nadra.
Uchunguzi, vipimo na matibabu hayalipishwi.
Chanjo ya Mpox
Chanjo inapatikana kwa matumizi ya kukabiliana na mpox. Chanjo hii inaweza kutolewa kabla au baada ya kuambukizwa. Chanjo hii hutolewa kwa watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa mpox.
Wakati mwingine chanjo hutolewa kwa watu ambao wamehatarishwa na maambukizi ya mpox. Hali hii hukadiriwa katika kila kisa. Kuchanjwa baada ya kuhatarishwa na virusi hivi hakutakuzuia kuugua ugonjwa huu, lakini kunaweza kutuliza makali ya dalili. Chanjo itakupa ulinzi bora zaidi ikiwa itatolewa ndani ya siku chache baada ya kuambukizwa, na pengine itakuwa na athari kndogo au ikose kuwa na dalili ikiwa itatolewa baada ya kupata dalili.
Safari
Kusafiri kwenda nchi zilizo na maambukizi ya mpox sio hatari kwa sasa.
Yeyote anayekusudia kusafiri au kukaa katika eneo lenye maambukizi yanayojulikana anapaswa:
- kufahamu kuhusu hali ya jumla mahali unakoenda na ufuate ushauri unaotolewa na mamlaka ya nchi husika
- kuepuka kugusana kimwili na mtu yeyote ambaye ameambukizwa
- kuepuka kuwa na wapenzi wengi/wa muda mfupi wa kimapenzi
- kuepuka kugusana kimwili na wanyama walio hai na waliokufa.
- kuepuka kula nyama ambayo haijapikwa vizuri na nyama ya wanyama pori
Kama kawaida, usafi wa mikono ni hatua muhimu ya kudhibiti maambukizi.
Taarifa zaidi kuhusu mpox zinaweza kupatikana kwenye tovuti ya Taasisi ya Afya ya Umma ya Norwe